President’s Office, Constitution, Legal Affairs, Public Service and Good Governance

THE LAW SCHOOL OF ZANZIBAR

Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake kuwa, iwapo dhana ya Uchumi wa Buluu itaeleweka vyema kutakuwa na nafasi nzuri ya kurekebisha na kuboresha sheria na taratibu za Mahakama

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kipazia kuashiria kuizindua Nembo ya Mahkama Kuu Tanzania wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma leo 23-1-2022 akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake kuwa, iwapo dhana ya Uchumi wa Buluu itaeleweka vyema kutakuwa na nafasi nzuri ya kurekebisha na kuboresha sheria na taratibu za Mahakama katika safari ya kuujenga uchumi wa Zanzibar.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria uliofanyika huko katika viwanja vya Nyerere Squire, Jijini Dodoma uliokwenda sambamba na uzinduzi wa Nembo pamoja na Bendera ya Mahakama.

Alieleza kwamba kwa lugha nyengine sheria na taratibu za Mahakama zilizopo lazima ziendane na mipango iliyopo ya Serikali yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia Uchumi wa Buluu.“Mimi binafsi nitafurahi sana kama wanasheria kutoka pande zote mbili za Muungano, mtakuwa na mijadala ya dhati kuhusu kwa kiasi gani, sheria na taratibu za kimahakama zinavyoweza kuboresha kwa lengo la kufanikisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ya ujenzi wa Uchumi wa Buluu”,alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alirejea kauli yake aliyoitoa mnamo Novemba 11.2020 katika hotuba ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pale aliposema kwamba Wazanzibari hawana budi kuigeuza bahari kuwa ndio shamba lao kwani huko ndiko fursa za ajira za Zanzibar mpya zilizopo ambapo pia, huo ndio msingi wa dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.Alisisitiza kwamba Zanzibar haikujaaliwa ardhi kubwa kwani ni nchi ya visiwa ambapo idadi ya watu wake imeongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 56 ambapo mwaka 1964 Wazanzibari walikuwa laki 3 tu ambapo hivi sasa wapo takriban 1.6. 

Katika hotuba hiyo Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa Wanasheria na wataalamu wa sheria, viongozi wa Mahkama na watumishi wa sekta za sheria kuielewa na kuifanyia kazi mipango mikuu ya uchumi wa Tanzania na kuwa huru kutoa ushauri wa kisheria Serikalini kwa lengo la kuifanikisha.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali zote mbili zinatambua kwamba zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwazo cha kufikia matarajio ya kiuchumi na ustawi wa jamii ambapo sheria hizo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko ili zifamikishe mipango ya uchumi wa kisasa.

Hivyo, aliwahimiza Wadau hao wa sheria, kutumia utaalamu wao kuzishauri Serikali zote mbili kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo zina kasoro na kufanya hivyo kwa maslahi mapana ya Tanzania na Watanzania wote.Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar dhamia ya Serikali ya kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia matumizi sahihi ya rasilimali za bahari au kama unavyofahamika Uchumi wa Buluu, ambazo ni jitihada za dhati kabisa za kujenga uchumi utakaowasaidia wananchi wa Zanzibar.

Alieleza kwa upande wa pili ambako kuna dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupunguza umaskini na kuwa na uchumi unaolingana na ushindani wa Karnr ya 21.Kutokana na juhudi hizo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa dhamira na jitihada hizo za Serikali zote mbili kutategemea uwezeshaji na mchango mkubwa wa sekta ya sheria na hasa kupata ushauri wa kutoka kwa wanasheria wa hapa nchini.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Sheria, kukumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji haki.

Alieleza kwamba amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria kwa vile anatambua kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni kuwepo wka vitendo vya rushwa, ubadhirifu,uzembe,kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria na kukiuka kwa maadili.

“Nafahamu kwamba sheria ina umuhimu mkubwa katika kujenga umoja wetu,amani yetu, udugu wetu, na pia mshikamano wetu, mafanikio ya kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji hutegemea kuwepo kwa misingi ya utawala wa sheria na uhuru wa Mahakama”, alisema Dk. Mwinyi.

Aidha,  Rais Dk. Mwinyi alieleza kuridhishwa na hatua ya ushirikiano iliyopo baina ya Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar ambapo uhusiano huo ni wa muda mrefu tokea mwaka 1965.“Nafurahi kuona kuwa ushirikiano huo unaendelezwa kwa kupeana uzoefu na utaalamu utakaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu hivyo natoa wito kuendeleza kwa lengo la kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji na kuongeza kasi ya ufanisi katika mahakama zetu”, alisisitiza Dk. Mwinyi.

Naye Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma alieleza kwamba wiki ya Sheria itakuwa na mambo mbali mbali ya kisheria hadi tarehe 29 na siku ya Sheria itakuwa Februari 1.2022 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.Aliwakaribisha wananchi kwenda katika maonyesho hayo yaliyozinduliwa na Rais Dk. Mwinyi ili waweze kupata mahitaji yao mbali mbali ya kisheria.

Jaji Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuimarisha sheria ikiwa ni pamoja na kuimarisha Uchumi wa Buluu ambao utahitaji mabadiliko ya Sheria huku akiahidi mashirikiano makubwa katika kuhalikisha dhana hiyo inafikia malengo yaliyokusudiwa sanjari na kuimarisha mashirikiano ya Kimahakama kati ya pande mbili hizo.

Pia, aliwasisitiza wananchi kuwa na utamaduni wa kujisomea hasa katika sheria huku wakiwataka wajitayarishe kwa kutumia mfumo wa “akili bandia” katika kutoa ushauri wa kisheria jambo ambalo linakwenda na wakati uliopo hivi sasa pamoja na kupunguza kharama za kuendeshea kesi.

Mapema asubuhi, Rais Dk. Mwinyi aliongoza matembezi ya kilomita saba yaliyoanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki, Jijini Dodoma na kupita katika maeneo mbali mbali na hatimae kuishia katika viwanja vya “Nyerere Square” ambapo Mama Maria Mwinyi nae alishiriki kikamilifu.

Baada ya kufika katika eneo hilo la uzinduzi huo, Rais Dk. Mwinyi alitembelea mabanda ya maonyesho pamoja na kuzindua rasmi bendera na Nembo ya Mahakama.