President’s Office, Constitution, Legal Affairs, Public Service and Good Governance

THE LAW SCHOOL OF ZANZIBAR

Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba iwapo jamii itazingatia mambo makubwa matatu likiwemo uadilifu, uaminifu na uwajibikaji basi mafanikio makubwa yatapatikana nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba iwapo jamii itazingatia mambo makubwa matatu likiwemo uadilifu, uaminifu na uwajibikaji basi mafanikio makubwa yatapatikana nchini.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika salamu zake alizozitoa mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Masjid Masoud uliopo Kiwengwa Kumbaurembo, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kuwa iwapo mambo hayo matatu muhimu yatafuatwa na wananchi wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya umma na wale wa sekta binafsi hatua kubwa ya maendeleo itafikiwa hapa nchini.

Alisema kuwa mambo hayo makubwa matatu ni miongoni mwa maagizo ya Mwenyezi Mungu ambapo pia ni hatua sahihi za kumfuata Mtume Mohammd (S.A.W), ambaye ni kigezo chema cha waumini wa dini ya Kiislamu. Akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Omar Abdi aliwaasa Waislamu kuwa waadilifu,waaminifu pamoja na wawe wawajibikaji katika majukumu waliyokabidhiwa.

Sheikh Omar alisisitiza kwamba ni vyema wale wanaopewa majukumu Serikalini na katika sekta binafsi wakawa waaminifu, waadilifu na wawajibikaji ili waweze kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Mapema waumini wa msikiti huo kwa niaba ya wananchi wenzao wa Kiwengwa walieleza kufurahishwa na uwamuzi wa Alhaj Dk. Mwinyi wa kusali nao pamoja katika msikiti huo huku wakieleza jinsi wanavyofarajika na uongozi wake ambapo pia, walitumia fursa hiyo kumuombea dua maalum ili Mwenyezi Mungu ampe nguvu zaidi za kuiongoza Zanzibar na kuiletea maendeleo endelevu.