Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa agizo la kuanza kazi Mahkama ya Rushwa Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi ameagiza taasisi zinazo husika na sheria kukamilisha mchakato wa utungaji wa sheria ili kuanza kazi kwa Mahkama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi kwa mwaka huu.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Sheria Zanzibar katika viwanja vya Mahkama kuu Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 07 Februari 2024.

Aidha Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha mhimili wa Mahkama na Taasisi zote za Sheria ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi, hatua hizo ikiwemo ujenzi wa majengo saba (7) ya Mahkama katika Mikoa na Wilaya Zanzibar, kuongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na Makadhi pamoja na kuboresha maslahi kwa Majaji, Mahakimu, Makadhi na watumishi wengine wa Taasisi za sheria ili kuongeza ufanisi.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amesema ustawi bora wa wananchi utategemea kuwepo kwa misingi imara ya kuheshimu haki za binadamu, utawala bora, uhuru wa Mahkama pamoja na sheria madhubuti zinazoilinda jamii dhidi ya aina zote za unyanyasaji.

Vilevile Rais Dk.Mwinyi ameipongeza Mahkama ya Zanzibar kwa kuanza mchakato wa kuboresha mfumo wa kieletroniki wa usikilizaji wa mashauri kwa msaada wa kitalaamu kutoka Mahakama ya Tanzania.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amezindua mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahkama (2024-2029) na kukabidhiwa ripoti ya utendaji kazi wa Mahkama ya mwaka 2023.